- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Hotuba ya Tatu Katika Kongamano: ‘Vijana Waislamu…Waanzilishi wa Mabadiliko Msingi’
Vijana Wanawakilisha Fursa Nzuri Zaidi
(Imetafsiriwa)
Dola, mashirika na mujtama za kibinadamu kwa muda mrefu zimekuwa zikishughulishwa na vijana – hili ni kweli leo na litaendelea kuwa kweli. Hii ni kutokana na yale yaliyomo katika rika hili kuhusiana na maendeleo ya kimwili na kiakili, yanayo ufanya umri huu kuwa tayari zaidi na kudhihirisha uchangamfu, nguvu, ubunifu, mafanikio, uongozi, ari, uvumilivu, ukarimu, kujitolea na maendeleo miongoni mwa sifa nyenginezo nzuri.
Katika thaqafa ya utandawazi tunayoishi ndani yake leo, inadhihirika kuwa neno ‘vijana’ linahusishwa katika akili za wengi na rika ambalo kiwango kikubwa cha anasa za kimwili hutafutwa, na mapenzi ya kupenda starehe, mzaha na kukesha (au kupoteza wakati) ndio mambo makuu ndani yake. Hili humulikwa na hamu ya ladha tofauti tofauti za michezo na sanaa. Ni rika hili la maisha ambalo kampeni ya mauzo ya Kampuni ya Coca Cola imelikusanya katika mwito wao wa mwaka huu. “Furahia Wakati”. Kampuni hii kubwa haikuandaa tu mwito huu pekee bali pia uliandamana na mbinu ya kimakusudi ya kuandika neno ‘Coca-Cola’, kwa muundo maalumu wa mduara mwekundu, muonekano wa kinje wa chupa hiyo na kikosi cha wasanii waliochukuliwa kupigia debe bidhaa hii. Kampeni ya vyombo vya habari ya kiulimwengu hufupisha ujumbe wake kwa kubeba maadili yake pamoja na filosofia ya kimagharibi kuhusu maisha kuhusiana na fungamano la mwanadamu na ulimwengu na maisha kwa sekunde kadhaa.
Vyombo vya habari vimemnyamazisha yule aliye matatani ili asalimu amri kwa ujumbe wake, aufuate na akubali yaliyomo katika jumbe zozote fiche. Mujtama katika biladi za Waislamu zimekuwa mujtama dhaifu za watumizi baada ya kuwa za uzalishaji na maendeleo. Tatizo haliko katika utamaduni wa matumizi pekee bali linapanuka hadi kwa ufisadi wa dola na mmomonyoko wa utambulisho. Vyombo vya habari vya runinga za Kiarabu, tangu mwanzoni mwake, vimemuonyesha kijana mdogo, akipambika na thaqafa ya kimagharibi katika mazungumzo, mavazi na mitizamo yake, kama mwakilishi wa maendeleo, aliye imara na mwenye furaha. Na huku yule aliye jifunga na Uislamu akionyeshwa kama mtu aliye na utambulisho usioimara na dhiki. Inawakilisha uvundo wa vyombo vya habari ambavyo havina utambuzi wa tofauti baina ya thaqafa ya kijana wa Kiislamu anaye tafakari, kuingiliana, kuzalisha na kufanya kazi ndani ya mpangilio wa Hukm Ash-Shar’i ili kuangaza njia yake, na baina ya “Furahia Wakati” ambayo ina ishi kwa muda huu tu huku ikifunga furaha kwa hisia za muda mfupi tu au kwa starehe au shibe ya mwili tu. Lakini ni upenyaji wa kithaqafa na utandawazi wa kifikra unao lazimishwa kwa nguvu juu yetu katika ulimwengu wa Kiislamu, unao tafuta kuzifanya fahamu zao kuhusu maisha zinazo chipuza kwengineko kando na mfumo wetu, Dini tukufu ya Uislamu, fahamu ambazo tunazi tabanni, kuzihami na kufanya kazi kuzimakinisha ndani ya mujtama zetu, hata kama zina kinzana na Aqeedah yetu na mtazamo wetu kuhusu maisha.
Vyombo vya habari hutoa taswira ya vijana kama rika lenye kupatiliza wasaa wa furaha na kujitolea nafsi zao kutafuta starehe huku wakati huo huo vikienda hadi kileleni kuhusu uhalisia wa masaibu ya vijana na matatizo yao kuhusiana na ukosefu wa ajira, muda wa faragha, upotezaji wakati, na shinikizo la mawazo. Vinawazingira vijana kwa sura mbovu, za uhalifu, mihadarati, muozo na akhlaqi fisidifu na kuziangazia tabia hizi na miondoko hii miovu hadi hili likageuka kuwa fikra ya kudumu inayo pachikwa juu ya vijana na kuongezea katika masaibu yao. vyombo hivi vya habari havijaribu kupanda sura nzuri inayo eneza matumaini na kuwaonyesha vijana kuwa umri huu maishani huwakilisha umri wa mafanikio, ufanisi na maendeleo. Na hilo ni kwa sababu vyombo hivi vya habari havifanyi kazi kuunyanyua Ummah huu.
Dada zangu waheshimiwa…
Leo ulimwenguni kwa kuwepo na maendeleo endelevu ya mbinu za uunganishaji na mawasiliano, uwezo wa mtu anaye miliki pesa na ushawishi wa kueneza fikra zake na kuzipigia debe umekuwa ni mkubwa. Runinga, redio na vyombo vya uandishi wa habari kwa aina zake tofauti tofauti vinapenya ulimwengu kuanzia sehemu yake ya mbali hadi sehemu yake ya karibu bila ya vizingiti vyovyote vikuu. Na hivyo vinaingia kila nyumba, sauti yake inasikika na kila sikio huku picha zake zikinasa kila jicho. Miundo hii ya vyombo vya habari inafanya kazi ya kutuma ujumbe kwa vijana katika hatua ya kuvuruga fikra. Hivyo haviwasilishi matatizo halisi ya maisha ya kila siku kwa njia ya umakinifu, huru na isiyo ya mapendeleo na endapo vitafanya hivyo basi itakuwa tu kwa lengo la kuchukua mwelekeo ule ambao mmiliki wa kituo au chombo cha habari, chochote kile, anaridhika nao. Vinafanya kazi katika kuamsha hisia (ghariza) na kuchochea hamasa na kuziamsha pasi na haja au manufaa yoyote yanayo tarajiwa, vikiwa havitoi chochote ila ushawishi muovu. Uharibu wa kimpango kupitia mechi za mpira za nchini, barani na kimataifa unaendelea takriban kwa njia ya kudumu. Mechi moja au shindano moja halimaliziki isipokuwa hufuatwa na jengine. Yeyote anaye okoka kutokana na mapenzi ya mpira huwasilishiwa miereka, mashindano ya magari na aina nyengizezo tofauti tofauti za upotezaji wakati. Hatusikii kutajwa kokote kwa ndugu zetu wa Cameroon, Ivory Coast au Gambia isipokuwa tu ndani ya muktadha wa Kombe la Afrika, kana kwamba mafungamano ya udugu yamefungika na misururu ya mpira!!
Yule ambaye havutiwi na michezo huambiwa ni lazima atawale ulimwengu kwa talanta zake za kindani katika uimbaji, uchoraji, uchezaji densi, maonyesho ya fesheni au uigizaji. Katika yote haya, yuko tayari kutumia pesa zake na wakati wake sambamba na watumizi wengine. Humhadaa na kumtongoza kutafuta talanta katika kujiachia na kufanya upuzi ili apoteze muda wake katika utafutaji wa kila kitu ambacho si chema. Vipindi vya runinga, mashindano na amali za kutafuta talanta za kisanii zimeshindwa kutatua misongo ya mawazo kwa wenye talanta za kikweli na wale wanaofanya kazi katika nyanja za utafiti wa kisayansi na uvumbuzi, na wale wanao fuzu. Vyombo vya habari huwapumbaza vijana huku uhamisho wa maarifa ukiendelea na maandamano ya wanasayansi na wale wale walio werevu wakiendelea kuondoka katika ardhi zilizo kataa kutambua kufaulu kwao na kuwavunja moyo kuhusiana na talanta zao.
Vyombo vya habari vimechafua sura ya mujtama ndani ya ardhi za Waislamu, kuharibu uhalisia wa kikweli na kufisidi mitizamo ya vijana huku vikimulika sura inayo gongana na uhalisia wa mujtamaa huu. Hivyo mwanamke akawa na ubinafsi na kuharibika na hana hamu nyengine isipokuwa kujipodoa uso wake, fesheni na vipindi vya upishi, huku mwanamume akiwa mbinafsi na kuzongwa na mahusiano mengi, huku mahusiano ya kijamii yakijengwa juu ya mada, manufaa na mitazamo ya kimakosa na hamasa za kirongo. Kufikia hapa naweza kukumbuka Kitabu cha Nyimbo cha Abu al-Faraj al-Isfahani, kitabu kilicho kusanya mashairi na maongezi yaliyo chafua historia ya zama za mwanzo za Uislamu na sura ya Zama za Dhahabu za hadhara ya Kiislamu iliyo yajaza macho na masikio na kuushangaza ulimwengu kwa jumla, alipoifunga kwa wafanyi kazi, makasri na mapungufu ya wafalme! Mujtama wa Waislamu ulionyeshwa kuwakilisha mujtama lemavu ambao pumbao na matamanio yalitawala ndani yake. Mujtama ulioishi kwa wasaa uliopo tu na ‘Kufurahia Wakati’. Hatupaswi kupuuza kuwa toleo la kwanza la kitabu hiki lilichapishwa Magharibi; watu wenye kasumba ya umamboleo walikuwa na hamu nacho na kusajili jeshi la wanaochunguza na wanaokashifu ili kunyanyua hadhi yake kwa malengo yao wenyewe.
Leo ulimwenguni, dola hucheza dori kubwa na msingi katika kuvisaidia vyombo vya habari katika kutekeleza dori yake. Hivyo basi, ni dola ndio inayotoa leseni kwa vyombo vya habari vya kibinafsi kutekeleza kazi yake na kuvisaidia kimaadili. Hii ni katika hali ambapo serikali sio mmliki halisi wa vyombo vya habari na msingi wa usaidizi wake. Kile ambacho vijana wetu wanafikishiwa katika nchi zetu za Kiislamu, kwa maana nyengine, ni mpangilio wa shambulizi lililo andaliwa linalotafuta kumakinisha fahamu ambazo zinagongana na mtazamo wetu kuhusu maisha. Wanawafanya vijana wetu, watoto wetu wenyewe, kutothamini juhudi zetu za haraka. Hizi ndizo juhudi zilizo anza kuleta matunda katika mchakato mkubwa wa mabadiliko na mapinduzi yenye baraka ya Ummah ambayo cheche yake ilianzia nchini Tunisia ‘kheri ya kijani’. Dola za kikoloni na walinzi wa utandawazi wamesimama nyuma ya mpangilio huu wa kifikra na kuusaidia kiakhlaqi na kimada. Wamiliki wa vituo vya runinga vya kibinafsi na vyombo vyenginevyo vya habari, ambao wametabanni fikra yao na kutembea barabara yao, wanawakilisha uongozi kuhusiana na utekelezaji wa shambulizi hili. Wanaosimama pamoja nao na kihakika mbele yao ni tabaka la viongozi katika nchi za Waislamu ambao wametabanni njia na fikra hizo hizo, kuwawezesha kueneza ufisadi wao na thaqafa mbovu tunayo ishuhudia leo.
Ujumbe wa vyombo vya habari unao kaririwa ni ‘Nyinyi tuachieni sisi na msiondoke kutoka katika kochi mwanana la mahmeli … Kwa nini mukimbilie kutenda ilhali mwaweza kuona, kujadili, kupika, kucheza michezo yote huku mukiwa mbele ya runinga? Kwa nini mukimbilie kutenda ilhali iko ndani ya uwezo wenu kutekeleza uhamasishaji wa kisiasa na kuingiliana na matukio, wakati ambapo mwaweza kukaa juu ya kochi lenu la mahmeli mukitazama runinga na kutumia mitandao ya mawasiliano?’ Ni kana kwamba vyombo vya habari vinawataka vijana kuachana na dori zao kama waanzilishi wa mageuzi ya kikweli na badala yake kukubali starehe bandia, kupoteza umri mzuri zaidi wa maisha yao na kutokubali jukumu lolote. Kana kwamba vijana hawaaminiwi na kustahiki kutekeleza hilo.
Dada zangu waheshimiwa…
Mtoto anapo lelewa katika kuzikumbatia simu za kisasa na michezo pasina nidhamu au udhibiti na kuwa kijana pasina mipaka ya kumfunza matendo yake na tabia zake, basi hapo haishangazi kwetu kuuona mpasuko ulioko sasa katika familia nyingi isipokuwa zile zilizo rehemewa na Mola. Baada ya nyuma kuwalea vijana wetu kutumia ujana wake kabla ya uzee wake, afya yake kabla ya maradhi yake na kufanya kwake bidii na kumsukuma katika ujana wake kupata (ujira) anapokuwa uzeeni na kuzunguka pamoja na gurudumu linalo saga la Uislamu, kunywa kutoka katika chemichemi ya elimu na kuongeza kupata kwake sifa na akhlaqi njema, baada ya hapo, tumekuja kuwafanya vijana kama yule anaye pitia mauti… Kijana yuko nyumbani kimwili tu lakini kiroho na kihisia hayuko, anaishi mbali na mnara wake halisi. Na hivyo kauli ya mshairi ikawa hakika:
Watu wamekufa lakini sifa zao zingali hai
Na watu wanaishi lakini ni miongoni mwa wafu
Vyombo vya habari na vituo vyake ni silaha iliyo na makali pande zote. Kwa upande mmoja vinafungua fursa kwa mtu na kumwezesha mtu huyo kuwasiliana, kusonga mbele na kunufaika, huku upande mwengine vina elekeza tafakari, ushawishi na tabia ya mtu na kumfanya mtu sponji la kunyonya kila fikra potofu na kila njia iliyo pitiliza… Anachorwa akiwa na mbawa pasina kuwa na nguvu yoyote (ya kukataa).
Ili kukabiliana na changamoto hii, ni muhimu kuuregelea na kuufahamu mtazamo wa Kiislamu kwa rika hili. Je, Ahkam zimewafafanua kwa kitu chochote cha kipekee? Na je, kuna msimamo wowote wa kipekee uliochukuliwa kuhusiana nao?
Ili kupambana na uwezo na shinikizo la vyombo hivi vya habari ambavyo vinauchafua utambulisho wa vijana Waislamu, ni lazima kuwe na nguvu imara sawia na zielekee dhidi yake. Inahitaji nguvu ya vyombo vya habari iliyo asisiwa juu ya misingi ya kimfumo inayopinga utenganishaji Dini na maisha, vyombo vya habari vilivyo asisiwa ndani ya upeo wa mpangilio kamili unao yachukulia matatizo ya Waislamu juu ya msingi wa Hukmu ya Shari’ah. Uchafuzi huu wa vyombo vya habari haiwezakani kupambana nao kwa vyombo hafifu vya habari vya Kiislamu vinavyo hutubia makundi maalumu na natija yake havina athari juu ya mujtama. Bali yahitaji mabadiliko ya kimsingi kwa mujtamaa yatakayo regesha mambo kuwa vile yanavyo stahili na kunali mizani ya usawa kati ya Aqeedah ya Ummah huu, thaqafa yake na hotuba za vyombo vya habari zinazo elekezwa kwake. Jambo hili laweza kuonekana kuwa kazi ngumu lakini kinacho lifanya kuwa rahisi ni Uislamu mtukufu kukitwa ndani ya maisha ya Waislamu.
Vyombo vitiifu vya habari vimepata ardhi yenye rutuba na kuwapata vijana wanaoteseka kutokana na utupu wa kifikra na kihisia, wakichukizwa na uhalisia wao na kuwa na kiu ya mabadiliko. Lakini, ni mapinduzi yanayo zunguka katika duara hafifu lisilo badilika… Ni mapinduzi yaliyo kosa lengo kwa hivyo ni muhimu kuangazia juu ya lengo hili ili mambo yaweze kuwekwa sawa… Ni muhimu kuamsha tafakari, kuimarisha utambulisho wa Kiislamu na kumakinisha maana ya ibada kwa Mwenyezi Mungu.
Wacha kilio kipae pambizoni mwetu na wacha kumkumbuka Mwenyezi Mungu kubakie kuzuri zaidi… Subhaanallah Wal-Hamdu Lillah Wa Laa Ilaaha Illallah Wallahu Akbar.
[وَالْبَاقِيَاتُ الصَّالِحَاتُ خَيْرٌ عِندَ رَبِّكَ ثَوَابًا وَخَيْرٌ أَمَلًا] “Na mema yanayo bakia ni bora mbele ya Mola wako Mlezi kwa malipo, na bora kwa matumaini” [Al-Kahf: 46].
[سُبْحَانَ رَبِّكَ رَبِّ الْعِزَّةِ عَمَّا يَصِفُونَ * وَسَلَامٌ عَلَى الْمُرْسَلِينَ * وَالْحَمْدُ لِلَّهِ رَبِّ الْعَالَمِينَ]“Ametakasika Mola wako Mlezi Mwenye enzi na yale wanayo mzulia. Na salamu juu ya Mitume. Na sifa njema zote ni za Mwenyezi Mungu Mola Mlezi wa walimwengu wote” [As-Safaat: 180-182].
Imeandikwa na
Huda Muhammad (Umm Yahya)