Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Kujitoa Muhanga Nafsi yako, Fedha zako na Wakati wako, ni moja katika sifa muhimu za Mbebaji Da'wah

(Imetafsiriwa)

Kubeba Da'wah ni kazi kubwa mno na ni njia iliyojaa magumu na matatizo, njia ambayo ilipitiwa hapo awali na Mtume wetu (saw) na Maswahaba zake (ra) na kuikabidhi wale ambao wameiamini Da'wah hii baada yao; ili kumlingania mwanadamu kutoka katika kuabudu viumbe na kumuita katika kumuabudu Muumba pekee. Hakuna ambaye anaweza kuyabeba magumu na matatizo ya njia hii isipokuwa mtu ambaye amejifunga, amejirekebisha na kujikuza mwenyewe kwa sifa za uzuri ambazo ni lazima awe nazo mbebaji Da'wah na sifa kubwa katika hizo ni 'kujitoa muhanga.'

Kujitoa muhanga inamaanisha: kupeana kitu pasi na kutarajia chochote, mfano kujitoa muhanga nafsi yako, fedha zako, kazi yako, muda wako, familia yako, elimu yako, cheo chako n.k mpaka mtu anahisi kuwa ana haki tu ya mahitaji msingi na si chengine chochote, kwa hiyo wanafanya bidii katika kujitoa muhanga pasi na kutafuta malipo ya kimada kutokana na mchango wao lakini wanatafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt) na kuinusuru Dini Yake.

Hakika, kufaulu hakufikiwi kwa matumaini na ubebaji Da'wah (ulinganizi wa Uislamu) umejengwa juu ya kila aina ya juhudi na kujitoa muhanga. Lau itafikia kuwa maradhi yametumwa juu ya wabebaji Da'wah ni jambo la kuendelea, basi itakuwa ni urongo kwa Da'wah ya haki kuweza kusimamishwa pasi na kujitoa muhanga.

Kujitoa muhanga kibinafsi ni sifa ambayo inatakiwa kubebwa na mbebaji Da'wah na lazima apambane na yatakayomfika katika njia hii; ya mateso, kukataliwa, kushtakiwa, kukatwa kwa mapato, kufungwa na kudhibitiwa katika nyanja zote za maisha. Anaweza hata kuuliwa. Na hadithi za Mitume na Manabii na maswahaba zao, ikijumuisha Mtume Muhammad (saw) na maswahaba zake, waliweka mfano mzuri kwetu sisi.

Kipenzi chetu Mtume (saw) hakuwa salama katika njia hii ya kuufikisha Uislamu kutokana na madhara ya wasioamini. Tokea alipopanda Mlima Safa na kuonya kabila lake waliokuwa karibu, alianza kupata madhara ya kila aina, walimzushia kuwa ni mchawi na mwenda wazimu baada ya kujulikana kuwa ni mkweli na muaminifu.  Yeye (saw) na maswahaba zake walipata madhara makubwa na walifikwa na mitihani mizito. Hivyo basi, Mtume (saw) alianza kujiwasilisha kwa makabila wakati wa msimu wa Hajj akiomba nusrah (ulinzi) ili aweze kulingania Dini ya Mwenyezi Mungu. Alikwenda Ta'if akitafuta lengo lake lakini alirudi huku miguu yake imejaa damu na kufurushwa, na alitengwa yeye, maswahaba zake na waliomuunga mkono katika majangwa ya Makkah kwa miaka 3 kiasi kwamba walikula majani ya miti kutokana na njaa.

Maswahaba wengi wa Mtume (saw) walionyesha juhudi na kujitoa muhanga kwa hali ya juu; Bilal, Sumayyah, Yasser na Ammar waliteswa vibaya mno kiasi kwamba Sumayyah (ra) na Yasser (ra) waliuliwa katika njia ya 'Aqeedah' walioshikamana nayo katika maisha, wakitafuta malipo ya Mwenyezi Mungu na pepo ambayo upana wake ni kama mbingu na ardhi. Maquraysh pia walimpiga Abdullah bin Mas'oud (ra) vibaya mno mpaka damu ikamjaa usoni mwake kwa kuwasomea aya alizoteremshiwa Mtume (saw). Alifurahi na kupata nishati kutokana na yale yaliyomfika, akijua fika kuwa aliyokumbana nayo yatahifadhiwa na Mwenyezi Mungu (swt); na ndiyo akasema "Wale maadui wa Mwenyezi Mungu hawajawahi kuwa duni thamani kwangu kuliko wakati huu, na lau mtataka nirudi tena kwao na nikawafanyie tena kesho.' Wakasema, 'La, inatosha kwako wewe. Umewafanya kusikiza ambacho wanakichukia." Mus'ab (ra) anatoka na kuacha nyuma starehe na kuhamia Madina kama mlinganizi wa Uislamu; Ali (ra) anajiweka katika hatari ya kuuliwa katika kitanda cha Mtume (saw) usiku wa Hijrah; Al-Baraa' alijitupa katika Bustani la Kifo kati ya maadui; kisha, Mwenyezi Mungu (swt) anawapa ushindi Waislamu kwa sababu yake, Abu Dardaa' aliwachana na biashara na kujifunga na ukuruba wa Mtume (saw); Khalid bin al-Waleed alikubali kuacha na cheo chake kwa kumuheshimu Ameer wa Waumini; Abu 'Ubaydah aliwacha cheo chake cha mkuu wa jeshi na kumpa Amr bin Al-Aas ili aweze kuwaunganisha Waislamu.

Da'wah yoyote ile husambazwa kwa juhudi za wafuasi wake, na Dini ya Uislamu haikusambaa kupitia utulivu wa mioyo na usalama wa nafsi. Dini ya Uislamu isingetufikia pasi na juhudi kubwa ya maswahaba wa Mtume (saw) na Waislamu waliokuja baada yao ambao waliacha nyumba zao, familia zao, watoto na biashara zao na kujitoa muhanga nafsi na mali zao kwa ajili ya hilo. Walifahamu kuwa wanabeba jukumu zito na adhimu kwa kuwa wao ni warithi wa Mtume (saw) katika ulinganizi wa Mwenyezi Mungu na utekelezaji wa hukumu za Mwenyezi Mungu ndani ya Dola ya Khilafah ili watu waweze kupata haki na huruma ya Uislamu na kuingia katika dini ya Mwenyezi Mungu kwa makundi. Hivyo basi, chochote kando na hili jukumu adhimu na kubwa ilikuwa ni jambo duni machoni mwao.

Ama kuhusu kuzitoa muhanga fedha zao, maswahaba wema ndio kiigizo chema kwa wabebaji Da'wah katika utoaji na ukarimu kuhusiana na mali zao. Ulinganizi wahitajia fedha na michango ili kuweza kutekeleza kazi zake na nani mbora au anyestahiki zaidi kuliko mbebaji Da'wah katika kuigharamikia Da'wah hii na kazi zake, kujifunga kuigharamikia kifedha kama anavyojifunga kwa watoto wake na walioko chini ya usimamizi wake na huwa mbioni kufanya khair ili kuitikia maneno ya Mwenyezi Mungu (swt): 

وَمَا تُنفِقُواْ مِن شَيۡءٖ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ يُوَفَّ إِلَيۡكُمۡ وَأَنتُمۡ لَا تُظۡلَمُونَ﴿

“Na mkitoa chochote katika Njia ya Mwenyezi Mungu mtarudishiwa, na wala nyinyi hamtadhulumiwa." [Al-Anfal: 60]

إِنَّ ٱلَّذِينَ يَتۡلُونَ كِتَٰبَ ٱللَّهِ وَأَقَامُواْ ٱلصَّلَوٰةَ وَأَنفَقُواْ مِمَّا رَزَقۡنَٰهُمۡ سِرّٗا وَعَلَانِيَةٗ يَرۡجُونَ تِجَٰرَةٗ لَّن تَبُورَ * لِيُوَفِّيَهُمۡ أُجُورَهُمۡ وَيَزِيدَهُم مِّن فَضۡلِهِۦٓۚ  إِنَّهُۥ غَفُورٞ شَكُورٞ﴿

"Hakika wale wanao soma Kitabu cha Mwenyezi Mungu, na wakashika Sala, na wakatoa kwa siri na kwa dhahiri katika tulivyowaruzuku, hao hutaraji biashara isiyo bwaga. Ili Yeye awalipe ujira wao kwa ukamilifu, na awazidishie kutokana na fadhila zake. Hakika yeye ni Mwenye kusamehe Mwenye shukrani." [Faatir: 29-30]

ٱلَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمۡوَٰلَهُم بِٱلَّيۡلِ وَٱلنَّهَارِ سِرّٗا وَعَلَانِيَةٗ فَلَهُمۡ أَجۡرُهُمۡ عِندَ رَبِّهِمۡ وَلَا خَوۡفٌ عَلَيۡهِمۡ وَلَا هُمۡ يَحۡزَنُونَ﴿

"Wale wanao toa mali zao usiku na mchana, kwa siri na dhahiri, wana ujira wao kwa Mola wao Mlezi; wala haitakuwa khofu juu yao, wala hawatahuzunika." [Al-Baqara: 274]

مَّثَلُ ٱلَّذِينَ يُنفِقُونَ أَمۡوَٰلَهُمۡ فِي سَبِيلِ ٱللَّهِ كَمَثَلِ حَبَّةٍ أَنۢبَتَتۡ سَبۡعَ سَنَابِلَ فِي كُلِّ سُنۢبُلَةٖ مِّاْئَةُ حَبَّةٖۗ وَٱللَّهُ يُضَٰعِفُ لِمَن يَشَآءُۚ وَٱللَّهُ وَٰسِعٌ عَلِيمٌ﴿

"Mfano wa wanao tumia mali zao katika Njia ya Mwenyezi Mungu ni kama mfano wa punje iliyo chipuza mashuke saba. Katika kila shuke zimo punje mia. Na kwa Mwenyezi Mungu humzidishia amtakaye, na Mwenyezi Mungu ni Mwenye wasaa na Mwenye kujua."  [Al-Baqara: 261]

Ziko aya nyingi katika Qur'an ambazo zinakokoteza kugharamia njia ya Mwenyezi Mungu. Zifuatazo ni Hadith za Mtume (saw) ambazo zinatilia shime kugharamika kwa njia ya Mwenyezi Mungu:

«ما من يوم يصبح العباد فيه إلا ملكان ينزلان، يقول أحدهما: اللهم أعطِ منفقًا خلفًا، ويقول الآخر: اللهم أعط ممسكًا تلفًا»

'Kila siku malaika wawili hushuka chini kutoka Mbinguni na mmoja wao husema: 'Ewe Mwenyezi Mungu! Mlipe kila mtu anayetoa katika njia Yako,' na malaika mwingine husema: 'Ewe Mwenyezi Mungu! Muangamize kila bahili'." (Bukharī: Na. 1374)

وعن أبي هريرة رضي الله عنه أن رسول الله صلى الله عليه وسلم قال: «قال الله: أَنْفِق يا ابن آدم أُنْفِق عليك» رواه البخاري ومسلم

Abu Hurairah amesimulia kwamba Mtume (saw) alisema: "Mwenyezi Mungu amesema, 'Tumia (katika sadaqa) Ewe mwanadamu, na Mimi nitatumia juu yako"  [Sahih Al-Bukhari na Muslim]

Maswahaba (ra), walifahamu maana yake kwa usahihi na kuzifanyia kazi, wakipelekea mifano yao kuwa ndiyo misingi na mwangaza unao muongoza yeyote anayeifuata njia yao. Abu Bakr Al-Siddiq (ra), alipeana mali yake yote kwa Mtume (saw) kwa sababu hiyo Mtume (saw) akamuuliza: "Umeiwachia nini familia yako?" Akajibu kuwa: "Nimewaachia Mwenyezi Mungu na Mtume (saw)." Uthman bin Affan (ra) akaligharamikia jeshi la al-Usra mpaka Mtume (saw) «ما ضر عثمان ما فعل بعد اليوم» “Hakuna kitakacho mdhuru Uthman baada ya aliyoyafanya leo”, na kukinunua kisima ndani ya Madinah kutoka kwa Myehudi mwanamume na kukitoa kama zawadi kwa wakaazi wa Madinah. Abu Talha aliitoa sadaqa mali yake iliyokuwa kipenzi Beeruha (bustani) kwa Mtume (saw) na kumwambia aitumie apendavyo baada ya kusikia aya ya Mwenyezi Mungu (swt):

لَن تَنَالُواْ ٱلۡبِرَّ حَتَّىٰ تُنفِقُواْ مِمَّا تُحِبُّونَۚ وَمَا تُنفِقُواْ مِن شَيۡءٖ فَإِنَّ ٱللَّهَ بِهِۦ عَلِيمٞ﴿

"KABISA HAMTAFIKIA wema mpaka mtoe katika vile mnavyo vipenda. Na kitu chochote mnacho kitoa basi hakika Mwenyezi Mungu anakijua." [Aal-Imran: 92]

Suhayb alipoteza mali yake yote kwa ajili ya kumfuata Mtume (saw) kwenda Madinah. Maswahaba wa Mtume (saw) walikuwa wakishindana  katika juhudi, ukarimu na kugharamia katika njia ya Mwenyezi Mungu, japo kwa kidogo, walikuwa na ari ya kutekeleza khair hii kwa kuwa walijua na walikuwa na yakini kuwa kila wanacho gharamikia kitahifadhi kwao na Mwenyezi Mungu (swt). Nguvu zao katika kuitumikia njia hii ya khair ili wafanya masikini miongoni mwa Maswahaba kumshitakia Mtume (saw) kwamba hawana chochote cha kutoa (sadaqa) na kwamba watu matajiri wanawashinda katika malipo. Muslim ameripoti kutoka kwa Abu Hurayrah (ra) aliyesimulia:

"أن فقراء المهاجرين أتوا رسول الله صلى الله عليه وسلم فقالوا: ذهب أهل الدثور بالدرجات العلى والنعيم المقيم، فقال: وما ذاك؟ قالوا يصلون كما نصلي، ويصومون كما نصوم، ويتصدقون ولا نتصدق، ويعتقون ولا نعتق، فقال رسول الله صلى الله عليه وسلم أفلا أعلمكم شيئًا تدركون به من سبقكم وتسبقون به من بعدكم؟ ولا يكون أحد أفضل منكم إلا من صنع مثل ما صنعتم، قالوا: بلى يا رسول الله، قال: تسبحون وتكبرون وتحمدون دبر كل صلاة ثلاثًا وثلاثين مرة"

"Masikini miongoni mwa Muhajirun walikuja kwa Mtume (saw) na kusema: Watu matajiri wana malipo yote; wanasali kama tunavyosali, wanafunga kama tunavyofunga na wana mali ya ziada ambayo wanatoa katika sadaqa; lakini sisi hatuna mali ambayo twaweza kutoa katika sadaqa." Mtume (saw) akawaambia: "Je nisiwafunze matamshi ambayo yatawafanya mufikie daraja ya wale wanaowashinda? Hakuna atakayefikia daraja yenu isipokuwa yule anayefanya kama nyinyi." Wakasema: "Kwa nini usitufunze, Mtume wa Mwenyezi Mungu? Akasema: "Mpwekesheni Mwenyezi Mungu (semeni: Mwenyezi Mungu ni Mkubwa) baada ya kila sala mara thelathini na tatu; na kumsifu Mwenyezi Mungu (semeni: Sifa Njema ni za Mwenyezi Mungu) baada ya kila sala mara thelathini na tatu; na kumtukuza (semeni: Utukufu ni kwa Mwenyezi Mungu) baada ya kila sala mara thelathini na tatu."

Mbebaji Da'wah anazoea kutoa sadaqa hata kama ni kidogo, wakati wa umasikini na uhitaji hususan wakati wa majanga na uadui ambao mahitaji ya Da'wah huzidi na huhitaji kujitoa muhanga zaidi, ataipa hadhi nafsi yake kwa kuisafisha kutokana na kuipenda Dunia. Mlango wa kuigharamikia Da'wah ambayo itarudisha tena utukufu kwa Waislamu na kurudisha tena ubwana wao katika haya maisha kwa mara nyingine tena ni moja ya milango bora ya khair na inajumuisha khair zote kwa uwezo wake Mwenyezi Mungu.

Ama kuutoa wakati muhanga, kama ilivyo muhimu kwa mbebaji Da'wah kutenga wakati wake kwa Da'wah usiku na mchana, na kutenga wakati wake bora ili kutekeleza amana aliyochagua kuibeba, kwa kuiamini kuwa ndiyo njia ya mwamko wa Ummah kutokana na madhara ya maisha haya mafupi, na kujitenga kwake na Mwenyezi Mungu na kutawaliwa na maadui. Mbebaji Da'wah huutoa muhanga wakati wake bora kwa ajili ya Da'wah hii na kuifanya kuwa ndiyo kipaombele katika maisha yake akitafuta radhi za Mwenyezi Mungu (swt) kama malipo, akiyatoa muhanga mapumziko yake na kulala kwake na hata kutoa muhanga wakati wa ajira yake kwa ajili ya Da'wah ya Mwenyezi Mungu, akiamini kuwa Mwenyezi Mungu (swt) anamuhifadhia muhanga wake kwa Siku ambayo hakuna pesa wala watoto watakaomnufaisha mtu na kwamba ataubariki wakati wake na vitendo vyake na rizq yake. Akiwa na yakini kwamba rizq yake itamfikia na haitopungua mfano wa punje –ima atafanya kazi kwa saa 20 au 8, au zaidi au chini kwa sababu rizq yake ishaandikwa na hatokufa kabla kuimiliki yote.

Ni imani hii inayomsukuma mbebaji Da'wah katika ulinganizi wa da'wah yake muda wote popote alipo: ajirani, nyumbani na familia yake, watoto wake na majirani, mjini mwake, anazungumza ukweli, anaamrisha mema na kukataza maovu, akigawanya muda wake kati ya ajira yake, masomo jumla na maalumu, akitembelea walengwa na kufanya kila ambalo Da'wah yamuhitajia kufanya. Daima yuko tayari kufanya lolote atakalo agizwa pasi na kusitasita au kuchelewa. Ni mchangamfu na mcheshi, mwenye moyo wa huruma kwa watu, mwenye kuwapendea khair, kujali manufaa na maslahi yao, yuko makini kuhakikisha ana wahamisha kutoka katika hali ya kumchukiza Mwenyezi Mungu (swt) hadi katika hali ya kumfurahisha Mwenyezi Mungu (swt). Anawapendea yale anayoipendea nafsi yake na kuwafikishia kile alichoruzukiwa na Mwenyezi Mungu katika ruwaza safi kiufahamu na kwa uwazi.

Hizi saa na dakika ambazo twaishi katika dunia ndiyo umri wetu; lazima tuzijaze ndani yake twaa na radhi za Mwenyezi Mungu (swt), tusizipoteze katika starehe, hata kama imeruhusiwa na kuacha yale ambayo Mwenyezi Mungu ametuamrisha juu yetu. Kila binadamu lazima ajiwekee mpangilio maalumu wa siku wa kazi yake (hususan mbebeji Da'wah) ili kujihesabu katika mapungufu yake kabla hajahesabiwa. Kurekebisha mapungufu aina yoyote katika haya maisha inawezekana, lakini Akhera hakuna kazi isipokuwa majuto na majonzi kutokana na uhalifu na hakika majuto yatakuwa hayasaidii.

فعن أبي برزة نضلة بن عبيد الأسلمي رضي الله عنه قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم: «لا تزول قدما عبد يوم القيامة حتى يسأل عن أربع: عمره فيمَ أفناه؟ وعن علمه فيمَ فعل؟ وعن ماله من أين اكتسبه؟ وفيمَ أنفقه؟ وعن جسمه فيمَ أبلاه» رواه الترمذي.

Abu Barza al-Aslami (ra) ameripoti kuwa Mtume (saw) alisema, "Miguu miwili ya mwanadamu haitoacha (kusimama mbele ya Mwenyezi Mungu) Siku ya Hukumu mpaka atakapoulizwa kuhusu mambo manne: kuhusu umri wake na alivyoutumia, elimu yake na alivyoitumia, mali yake na alivyoichuma na alivyoitumia; na mwili wake namna alivyoutumia. [Sahih, imeripotiwa na At-Tirmidhi]

وعن ابن عباس رضي الله عنهما قال: قال رسول الله صلى الله عليه وسلم لرجل وهو يعظه: «اغتنم خمسًا قبل خمس: شبابك قبل هرمك، وصحتك قبل سقمك، وغناءك قبل فقرك، وفراغك قبل شغلك، وحياتك قبل موتك» رواه الحاكم بالمستدرك.

Ibn Abbas ameripoti kuwa Mtume (saw) alisema, "Patiliza mambo matano kabla matano: ujana wako kabla uzee wako, afya yako kabla maradhi yako, utajiri wako kabla umasikini wako, muda wako uliokuwa na nafasi nao kabla kazi zako, uhai wako kabla mauti yako." [Imesimuliwa na Al-Hakim katika al-Mustadrak]

Ni wazi na inaonekana kuwa Mwenyezi Mungu (swt) alibariki zama za wanavyuoni wa kweli, waliweza kufanya mambo makubwa pasi na kuyadhania kimahesabu ya kimada, naye Mwenyezi Mungu (swt) akayabariki maneno, vitendo na vitabu vyao na wakafikia upeo wa kunufaisha na kuathiri ambao haikuwahi kutokea kwao na wameutoa muda wao muhanga mkubwa. Natija ya muhanga katika hali na juhuzi zote ni malipo, manufaa na muongozo asiodiri mtu isipokuwa Mwenyezi Mungu (swt) ndiye anayejua kama alivyosema Mtume (saw):

«من دعا إلى هدى كان له من الأجر مثل أجور من تبعه، لا ينقص ذلك من أجورهم شيئًا»

"Yeyote anayelingania katika uongofu atakuwa na malipo sawa na wale wanaomfuata, bila kupunguziwa chochote katika malipo yao."

وعنْ أَبِي مسعود الأنصاري رضي الله عنه قَالَ: قال رَسُولُ اللهِ صلى الله عليه وسلم: «مَنْ دَلَّ عَلَى خَيْرٍ فَلَهُ مِثْلُ أَجْرِ فَاعِلِهِ»

Abu Mas'ud Al-Ansari (ra) ameripoti: "Yeyote anayemuongoza mtu katika khair atalipwa malipo sawa na yule anayetekelez kitendo hicho cha khair."

وقال رسول الله صلى الله عليه وسلم لعلي رضي الله عنه يوم فتح خيبر في حديث طويل: «فوالله، لأن يهدي الله بك رجلًا واحدًا خير لك من أن يكون لك حمر النعم»

Mtume (saw) alimwambia Ali (ra) siku ya kuifungua Khaybar: "Kwa uwezo wa Mwenyezi Mungu, lau mtu mmoja ataongozwa na Mwenyezi Mungu kupitia wewe, itakuwa bora kwako kuliko zaidi ya ngamia wekundu." 

Mwisho kabisa, kwa kuwa Da'wah imekitwa katika kujitoa muhanga, basi kila mbebaji Da'wah anafahamu nini la kufanya.

Ewe Mwenyezi Mungu, tunakuomba utupe utambuzi wa yale yaliyo ya sawa, khair, mbinu zilizo bora katika mazungumzo na vitendo na tufanye sisi tuwe ni wenye kusikiza kwa makini yale yote yanayosemwa na kufuata yale yaliyo bora na tufanye sisi kuwa ni funguo za khair na kufuli za maovu na tupe zawadi ya Fadhila Zako, Khair na Ukarimu wa Khilafah kwa njia ya Mtume, Ewe Bwana Mwenye Nguvu na Utukufu. Maombi yetu ya mwisho ni Alhamdulillahi Rabbil ‘Aalamin, Amani na Baraka za Mwenyezi Mungu ziwe juu ya Mtume wetu Muhammad, familia yake na maswahaba zake.

Chanzo:  Jarida la Al-Waie, Toleo 387, Rabi’ul Akhir 1440 H – Disemba 2018 M

Imebadilishwa mara ya mwisho mnamoJumapili, 12 Aprili 2020 06:51

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu