Jumatatu, 21 Jumada al-thani 1446 | 2024/12/23
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Udhalimu wa Kidemokrasia katika Ugavi wa Mapato

Habari:

Pendekezo juu ya ugawanyaji wa mapato baina ya kaunti ambalo litayapa mapendeleo makubwa maeneo yaliyo na idadi kubwa ya watu limesababisha mgawanyiko mkubwa katika bunge la Seneti. Kushindwa kwa Seneti kukubaliana juu ya msingi wa tatu wa mbinu ya ugawanyaji mapato natija yake imezitumbukiza kaunti katika kina zaidi cha mgogoro wa kifedha kwani sasa itachukua muda mrefu zaidi kwa kaunti kugawanya Sh316.5 bilioni zilizotengewa kama mapato ya ugavi adilifu katika mwaka wa fedha wa 2020/21. [Daily Nation]

Maoni:

Kikatiba, ugavi wa mapato ni kazi ya Tume ya Ugavi wa Mapato (CRA) ambayo ni kutoa mapendekezo kuhusiana na msingi wa ugavi adilifu wa mapato yaliyo kusanywa na serikali ya kitaifa baina ya serikali ya kitaifa na za kaunti; na baina ya serikali za kaunti.

Tangu kuanza kwa mwaka wa fedha Julai 2020, kumekuweko na mjadala mkali juu ya ugavi wa mapato ya kusambazwa kwa serikali za kaunti. Kizingiti kilicho katika Bunge la Seneti ambalo limewajibishwa, kupitia azimio, kuamua msingi wa kugawanya baina ya kaunti mgao wa mapato ya kitaifa ambayo hutengwa kila mwaka kwa ngazi ya serikali za kaunti. CRA iliunda mbinu mpya ya kugawanya mapato kwa msingi wa majukumu, idadi ya watu na viwango vya umasikini. Hapo awali, idadi ya watu, umasikini na ukubwa wa eneo vilikuwa ndio kichocheo cha ugavi wa mapato. Lakini, katika mbinu iliyofanyiwa marekebisho, kaunti zilizo na idadi kubwa ya watu lakini eneo dogo zitapata pesa zaidi kuliko zile zilizo na idadi ndogo ya watu lakini eneo kubwa.

Mvutano uliopo sasa ulioshuhudiwa kwa wanasiasa wote na mashirikiano nchini Kenya juu ya ugavi wa mapato kwa kaunti 47 umedhihirisha sura halisi ya udhalimu wa idadi katika nchi za kidemokrasia. Walo wengi ndio ufunguo wa kudumisha mamlaka ya kisiasa katika demokrasia, na hivyo basi kupata hisa ya windo la simba katika ile inayoitwa keki ya kitaifa (ugavi wa mapato). Huku kaunti zilizo dhaifu Kidemokrasia zenye idadi ndogo ya wakaazi zikicheza dori kwa kujaribu kusukuma ugavi adilifu wa mapato wenye kuakisi maendeleo sawa na ya kudumu katika utoaji huduma pamoja na uwekezaji wa rasilimali, juhudi hii ni mithili ya kukata kiu kwa kufukuzia mangati.

Huku siasa za 2022 zikizingua, ni wazi kwamba mpango wa mbinu ya kuzigawanya Sh316.5 bilioni ($31 milioni) umevurugwa na wanasiasa ili kutumikia matarajio yao ya kisiasa. Siasa za ubinafsi zilizoundwa na mfumo fisidifu wa kirasilimali huyatanguliza maslahi ya mtu binafsi juu ya raia wa kawaida. Hili linaelezea wazi kuwa ugavi wa mapato ni chombo cha kufikia malengo ya kisiasa na sio kuwanufaisha umma kama inavyo dhaniwa. Fauka ya hayo, ugavi wa mapato chini ya serikali za kirasilimali hutia vikwazo zaidi vya kiuchumi na kifedha kupitia kutoza kodi vikimu maisha (bidhaa na huduma).

Ukusanyaji na ugavi wa mapato ya dola chini ya Khilafah huunda mazingira mwanana kwa raia kufikia ustawi wa kiuchumi. Katika Uislamu, imeharamishwa utozaji kodi vikimu maisha kwani hili husababisha kuenea kwa umasikini. Ama ukusanyaji wa mapato na ugavi wake, haya yameainishwa waziwazi na Shariah ambayo imeonyesha mipaka wazi baina ya mali ya dola, mali ya umma na mali ya kibinafsi. Hakuna nafasi kwa kampuni za kibinafsi kumiliki kipekee manufaa kutoka kwa rasilimali za umma kama inavyo onekana katika uchumi wa kirasilimali, kwani Uislamu umefafanua maumbile ya mali za umma na ugavi wa mapato yake yaliyozalishwa na hivyo basi kuunda uchumi madhubuti na wenye nguvu.

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Office of Hizb ut Tahrir na
Ali Omar
Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Kenya

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu