- |
- Kuwa wa kwanza kutoa maoni!
- ukubwa wa font punguza ukubwa wa font zidisha ukubwa wa font
بسم الله الرحمن الرحيم
Kauli za Rais Erdogan kuhusiana na Heshima ya Kieneo ya Syria, Ambazo Amezitoa kwa Kila Fursa, Zinamaanisha Kuukubali kimyakimya Utawala wa Assad, ambao Umekuwa Ukiwachinja Kikatili Waislamu kwa Miaka Mingi
(Imetafsiriwa)
Habari:
Waziri wa mambo ya nje Mevlut Cavusoglu alisema, "Operesheni hizi zina umuhimu katika suala la heshima ya kieneo ya Syria na Iraq. Endapo hatungefanya hivi, sio DAESH wala YPG-PKK ingeondolewa. Hatuwezi kubaki walegevu dhidi ya mashambulizi. " (Mashirika ya Habari)
Maoni:
Erdogan, katika taarifa mmoja baada ya kikao cha mwisho cha baraza la mawaziri alisema, "Tutaanza kuchukua hatua mpya hivi karibuni kuhusiana na sehemu zinazokosekana za kazi ambayo tumeanza ya kubuni maeneo salama yenye kina cha kilomita 30 kwenye mipaka yetu ya kusini. Maeneo ambayo ndio kitovu cha mashambulizi ya mara kwa mara, uhangaishaji na mitego kwa nchi yetu na maeneo salama yako juu ya vipaumbele vyetu vya operesheni. Punde tu Vikosi vyetu vya Jeshi la Uturuki, ujasusi na usalama vitakapokamilisha maandalizi yao, operesheni hizi zitaanza."
Kwa upande mwingine Waziri Çavuşoğlu alitoa sentensi muhimu ifuatayo katika kipindi cha televisheni alichohudhuria, akikumbusha kuwa wanafanya mazungumzo na Iran kwa ajili ya kuwaondoa magaidi katika eneo hilo.
"Pia tutaunga mkono operesheni ambayo serikali (Damascus) itatekeleza. Lakini serikali hiyo haipaswi kuuchukulia upinzani wa wastani kama magaidi vilevile...”
Siku chache kabla ya kauli hii ya Waziri Mevlut Cavusoglu, akijibu maswali ya waandishi wa habari kwenye ndege akirudi Sochi, Rais Erdogan alisema kwamba Putin alimwonyesha Assad anwani moja ya Syria, akisema: "Hapa anatudokezea kwamba itakuwa sahihi zaidi ikiwa munapendelea njia ya kutatua haya pamoja na serikali iwezekanavyo'. Pia tunasema kwamba hivi sasa shirika letu la kijasusi tayari linaendesha maswala haya na ujasusi wa Syria, lakini suala zima ni kupata matokeo," alisema.
Erdogan aliendelea, "Ikiwa upelelezi wetu unafanya kazi hii na ujasusi wa Syria, na licha ya hayo, bado kuna mashirika ya kigaidi yanayopatikana huko, tunasema kwamba munahitaji kutuunga mkono katika suala hili. Pia tuna makubaliano juu ya suala hili."
Kwa hakika, mkutano wa maafisa wa kijasusi wa Uturuki na Syria sio wa kwanza. Mnamo Januari 2020, mkuu wa Ujasusi wa Kitaifa wa Uturuki, Hakan Fidan na mkuu wa ujasusi wa Syria Ali Mamluk, walikutana jijini Moscow. Lakini, PYD, ambayo Erdogan anaiona kama shirika la kigaidi, ilifungua afisi rasmi huko Moscow mnamo 2016.
Inajulikana kuwa Erdogan alijadili masuala ya uwezekano wa operesheni ya kijeshi nchini Syria au kaskazini mwa Syria na rais wa Urusi Putin wakati wa ziara yake ya hivi karibuni jijini Sochi. Inajulikana kuwa Iran na Urusi hazikuidhinisha operesheni hii ya kijeshi katika mkutano wa Tehran uliofanyika kati ya Uturuki, Iran na Urusi.
Ingawa kuna mizozo kadhaa kati ya dola hizi tatu kuhusu utatuzi wa mgogoro wa Syria, mhusika mkuu nchini Syria ni Marekani. Dola hizi tatu zinafanya kazi ndani ya mzunguko wa Amerika nchini Syria na zinaongoza vita vya wakala kwa niaba ya Amerika. Marekani inatumia dola hizi kama kichocheo cha maslahi yake ya kisiasa ili kutekeleza maamuzi yaliyochukuliwa katika Mkutano wa Geneva wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa mwaka 2012 na kufikia suluhu ya kudumu ya kisiasa nchini Syria. Operesheni zote za kijeshi ambazo serikali ya Chama cha AK imezifanya nchini Syria hadi sasa kwa maelekezo na idhini ya Marekani zote ni operesheni za kumlinda Assad katili na kuyachukua tena maeneo yaliyopotea kwa utawala huo. Kwa kuongeza, matamshi kuhusu heshima ya kieneo ya Syria, ambayo Erdogan na mamlaka za serikali sasa wanayatoa katika kila fursa, yanamaanisha kuukubali kimyakimya utawala katili wa Assad, ambao umekuwa ukiwachinja kikatili Waislamu kwa miaka mingi.
Hata hivyo, Erdogan anataka kuingia katika uchaguzi ujao wa Rais wa 2023 na mkono wenye nguvu. Inaonekana Erdogan na chama chake wamepata hasara kubwa ya kura kutokana na mzozo wa kiuchumi nchini Uturuki. Kura nyingi za maoni ya umma zilizofanywa pia zinathibitisha hili. Uchaguzi wa 2023 ni muhimu kwa Erdogan. Chaguzi hizi ni muhimu sana sio tu kwa Erdogan, lakini pia kwa Amerika, ambayo anaitegemea. Amerika haitaki kukipoteza kile ilichokipata hadi sasa kupitia Erdogan. Itakuwa sawa kutathmini kila hatua ambayo Erdogan atachukua ndani na nje katika mwelekeo huu.
Ili kuimarisha mkono wa Erdogan ndani pamoja na nje na kuongeza umaarufu wake, Amerika iliipa Uturuki dori ya kutatua suala la mgogoro wa nafaka kati ya Urusi na Ukraine. Amerika pia ilitaka kuimarisha mkono wa Erdogan tena kwa kuhalalisha uwepo wa Mayahudi na nchi kama vile Imarati, Misri, nchi za Ghuba na Saudi Arabia, ambapo serikali hiyo ilipitia migogoro ya kidiplomasia kwa muda. Tena, Marekani sasa inaitaka Uturuki kufanya mazungumzo ya kidiplomasia na Syria ili kurekebisha uhusiano wa Uturuki na Syria na kutatua mgogoro wa Syria haraka iwezekanavyo.
Kwa upande mwingine, Rais Erdogan alianzisha Muungano wa Watu na MHP (Chama cha Vuguvugu la Wazalendo) baada ya jaribio la mapinduzi la Julai 15. Lakini muungano huu na wazalendo wa Kituruki uliwakasirisha na kuwatenga wapiga kura wa Kikurdi ambao hapo awali walimpigia kura. Matamshi ya mara kwa mara ya Erdogan kuhusu operesheni ya kijeshi inayokaribia nchini Syria ni kauli inayolenga umma, na hasa wazalendo ambayo haiendi zaidi ya utekelezaji. Kwa hivyo, Erdogan yuko katika shida ya kuunganisha tena mizizi yake mwenyewe na wapiga kura wa wazalendo ambao wamejitenga naye kutokana na mgogoro wa kiuchumi. Ni kubembeleza hisia zao.
Matokeo yake, pasi na kujali tatizo la Erdogan ni nini, kuna ukweli unaojulikana kwamba amewasaliti Waislamu wa Palestina, Turkestan Mashariki, Arakan na Syria. Sio tu kwamba ameupa kisogo Ummah ili kuitambua Marekani na maslahi yake binafsi, bali kinyume chake, ameudunga kisu cha mgongo Ummah.
Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na
Yılmaz ÇELİK