Afisi ya Habari
Tanzania
H. 23 Rajab 1439 | Na: 1439/02 |
M. Jumanne, 10 Aprili 2018 |
Taarifa kwa Vyombo vya Habari
Waislamu na Wanadamu kwa Jumla ni Wakati wa Kukumbuka Siku Hii
Mwishoni mwa mwezi huu mtukufu wa Rajab, mataifa ya kirasilimali na ya kikoloni baada ya kupangiliwa vizuri kwa njama na mikakati ya muda mrefu yalifaulu kuivunja Dola ya mwisho ya Kiislamu ya Khilafah Uthmaniya ambayo makao yake makuu yalikuwa nchini Uturuki, tukio ambalo lilifikia kileleni mwake mwishoni mwa Rajab 1342 H / Machi 1924 M.
Kwa kuwa Uislamu umeletwa kama rehma kwa wanadamu wote, dola ya Khilafah vilevile ni nuru na ukombozi kwa Waislamu na wanadamu kadhalika. Hivyo basi, kuvunjwa kwake kuliacha athari kubwa mno, wasiwasi na maumivu kila mahali. Kwa maana nyingine, kuvunjwa kwa Khilafah kumewapelekea Waislamu na wanadamu katika misururu ya mateso, vilio, majanga nk.
Kuvunjwa kwa Khilafah kumewapelekea Waislamu kupata hasara kubwa kupitia kutawaliwa juu yao kwa nidhamu nyingine isiyokuwa Uislamu. Hili limewaweka mbali na faradhi muhimu mno na ibada tukufu mbele ya Muumba wao.
Vilevile, wameshindwa kuishi chini ya kivuli kimoja imara, (dola ya Khilafah), inayo waunganisha kama Ummah mmoja bila ya kujali rangi zao, maeneo yao au mistari iliyo chorwa na wakoloni (mipaka ya kitaifa).
Zaidi ya hayo, wameshindwa kuishi kwa amani, utulivu na furaha, na badala yake wanaishi kwa hofu, mateso, mauaji, uvamizi, unyanyasaji usio na haja, wanaishi pasi na mtetezi na msimamizi wa kweli. Kubwa zaidi, Waislamu na Uislamu unadhihirishwa na mataifa ya kikoloni ya kimagharibi hususan Marekani kama maadui wa wanadamu ulimwenguni.
Ama wasiokuwa Waislamu, kuvunjwa kwa Khilafah kumewanyima fursa ya dhahabu ya kutawaliwa kwa Uislamu; mbali na ukweli kuwa kamwe hawange lazimishwa kusilimu. Kutokana na kutekelezwa kwa utawala wa Uislamu, wangeshuhudia nguvu ya Uislamu kifikra na kivitendo upande wa uadilifu, usawa na haki. Kupitia utawala huo, pia wangepata fursa ya kutofautisha baina ya nidhamu ya kiimla ya kisekula ya kileo ya kidemokrasia inayozitenga dini na kutegemea nidhamu na kanuni zilizotungwa na wanadamu, na utawala na nidhamu ya Kiislamu inayo afikiana na uhalisia na umbile la mwanadamu.
Vilevile, wameshindwa kuishi chini ya dola inayo amiliana na kuwazingatia raia wake wote kwa msingi mmoja pekee wa uraia, sio dini, rangi wala kabila. Kwani Khilafah katika historia ilifaulu kuwafinyanga aina zote za watu kama taifa moja bila ya ubaguzi.
Fauka ya hayo, wamekosa fursa ya dini yao kulindwa, kinyume na nidhamu ya leo ya kidemokrasia / urasilimali ambapo dini hulazimishwa na kusimamiwa kwa mujibu wa matamanio na matakwa ya kidemokrasia, kufikia hadi kuwalazimisha kuhalalisha maovu na vitendo vya aibu kama liwati.
Kwa kutamatisha kama Waislamu, ni lazima waendelee kufanya ulinganizi (da'wah) ya kusimamisha tena Khilafah Rashidah, wakilenga kusimamisha dola katika mojawapo ya biladi kubwa za Waislamu kwa kutumia njia ya Mtume Muhammad (saw) ambayo haihusishi utumiaji wa nguvu, silaha au ghasia.
Pia ni wakati sasa kwa wasiokuwa Waislamu kuusoma Uislamu kwa undani na kuutafiti kama nidhamu mbadala, yenye matunda, adilifu na ya kweli, hususan kwa kuwa hali ya ulimwengu leo ambapo urasilimali na nidhamu yake ya kisiasa imesababisha maangamivu makubwa na mateso kwa wanadamu.
Masoud Msellem
Mwakilishi kwa Vyombo vya Habari wa Hizb ut Tahrir Tanzania
#SimamisheniKhilafah
Hizb-ut Tahrir: Afisi ya Habari Tanzania |
Address & Website Tel: +255778 870609 |
E-Mail: mediarep@hizb.or.tz |