Jumatatu, 23 Jumada al-awwal 1446 | 2024/11/25
Saa hii ni: (M.M.T)
Menu
Main menu
Main menu

بسم الله الرحمن الرحيم

 Fedheha kwa Michakato ya Kulinda Amani ya Umoja wa Mataifa Nchini Congo (DRC)

(Imetafsiriwa)

Habari:

Jumatatu tarehe 25/08/2022, wakaazi wa mji wa mashariki wa Beni katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) walivamia afisi za Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Kuleta Utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (UN-MONUSCO) wakiandamana kutokana na kushindwa kwa miradi hiyo ya Umoja wa Mataifa kulinda maisha yao.

Maoni:

Tangu mwaka 1999, Umoja wa Mataifa kupitia Azimio la Baraza la Usalama nambari 1379 lilianzisha kikosi kwa ajili ya kufuatilia na kuangalia mchakato wa amani kutokana na vita vya pili vya Congo (DRC). Mchakato wa kikosi hicho uliitwa Ujumbe wa Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (MONUC-Mission de l’Organisation des Nations Unies en République démocratique du Congo).

Mnamo Julai mwaka 2010, MONUSCO ambayo ni Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa kuleta utulivu katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo ulishika hatamu badala ya mchakato wa awali wa MONUC, na unaendelea mpaka hivi leo.

Miradi yote miwili ya MONUC na MONUSCO ikichukuliwa ati ndio michakato mikubwa zaidi ya vikosi vya Umoja wa Mataifa vya kulinda amani nchini Congo (DRC) imekuwa ikijihusisha na unyonyaji wa kingono na udhalilishaji unaofanywa dhidi ya wanawake na watoto. Imeripotiwa katika kisa kimoja kuwa mtoto mdogo wa kike mwenye miaka kumi na sita alibakwa na “walinda amani” watano wakati akikusanya chakula (Shirin Bakhti, Sexual Exploitation and Abuse by UN Peacekeepers, 2019). Uovu ulioje wa watu hawa!

Licha ya ubakaji unaofanywa na vikosi vya walinda amani wa Umoja wa Mataifa nchini Congo (DRC), hali iliyopelekea nchi hiyo kubandikwa jina la ‘jiji la ubakaji’, walinda amani hao nchini Congo (DRC) pia wanajihusisha na biashara ya ngono na ukatili wa kijinsia kwa wanawake na watoto.

Kwa mujibu wa shirika lisilo la kiserikali la “Save the Children”, katika ripoti yake ya mwaka 2008 iliyoitwa “No one to Turn to” yaani “Hakuna wa kumkimbilia” ilithibitisha kuwa watoto wadogo wenye miaka sita wanafanya biashara ya ngono na wafanyikazi wa misaada na walinda amani kwa mabadilishano ya chakula, pesa, na vitu vidogo vidogo vya matumizi. Jumla ya malalamiko 623 ya unyonyaji wa kingono na udhalilishaji dhidi ya MONUSCO yalifunguliwa kati ya mwaka 2004-2005 pekee.

Ni wazi kuwa walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa wanatumia vibaya hali ya ufukara na ugumu wa maisha nchini Congo. Bila ya aibu wafanyikazi hao wa Umoja wa Mataifa badala ya kutekeleza ipasavyo jukumu lao la kulinda amani, wanajikita katika ukatili wa kingono kwa watoto wa kike wasio na hatia ambao baadhi ni wadogo sana wakiwa na miaka sita, kwa kuwalaghai na kuwahonga pesa na vitu vingine katika mahitaji msingi kama chakula, nguo nk.

Zaidi ya hayo, walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa wameripotiwa kuua watu wasio na hatia mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo mwaka 2013, huku katika maandamano ya karibuni zaidi ya raia 15 wameuawa na 50 kujeruhiwa.

Michakato hii ya amani hutarajiwa kuwalinda raia na ustawi wao lakini badala yake inawaua. Raia wanalaumu na kuonesha kutoridhishwa kutokana na kushindwa kwa vikosi hivi kutekeleza majukumu yao ipasavyo, badala yake vimekuwa vikijihusisha kuwabaka, kupora na hata kuwaua.

Mgogoro nchini Congo (DRC) ni kati ya mataifa ya Ulaya hasa Uingereza dhidi ya Amerika juu ya rasilimali nyingi za Congo ambazo ni pamoja na dhahabu na almasi. Wakati Amerika inaitumia Rwanda, Uganda na Burundi zinazoongozwa na Watutsi wanaoungwa mkono na Amerika, Uingereza nayo inatumia nchi za kusini mwa Afrika zilizoko katika mrengo wake kama Zimbabwe, Zambia na Afrika Kusini kudhibiti mienendo ya Amerika.

Wanaoitwa eti “walinzi wa amani wa Umoja wa Mataifa hawajawahi kufanya chochote katika kusaidia na kustawisha mchakato wa amani nchini Congo, na kiuhalisia uwepo wao sio kwa lengo hilo. Jukumu lao kubwa ni kulinda maslahi na miradi ya uwekezaji wa mabwana zao mabepari wakoloni wa Kimagharibi, wa kihakikisha wananyonya kwa haraka na kwa usahali bila bughudha yoyote utajiri mkubwa wa rasilimali za Congo (DRC). Kwa hiyo, isitarajiwe kwa makundi haya ya kishenzi yenye silaha kwa jina la walinzi wa amani, kuleta amani yoyote nchini Congo (DRC) au popote, kwa kuwa wao pia ni sehemu ya tatizo.

Ili kuleta amani ya kweli na kusaidia watu wa Congo (DRC), Afrika na nchi zinazoendelea kiujumla, tunahitaji kuondoa katika mizizi yake mfumo wa ubepari na kurejesha tena serikali ya kiulimwengu ya Kiislamu (Khilafah) itakayowalinda Waislamu na dunia nzima dhidi ya aina zote za unyonyaji na dhulma.

Mwenyezi Mungu (swt) anasema:

[يَهْدِي بِهِ اللَّهُ مَنِ اتَّبَعَ رِضْوَانَهُ سُبُلَ السَّلَامِ وَيُخْرِجُهُم مِّنَ الظُّلُمَاتِ إِلَى النُّورِ بِإِذْنِهِ وَيَهْدِيهِمْ إِلَى صِرَاطٍ مُّسْتَقِيمٍ]

“Mwenyezi Mungu huwaongoa wenye kufuata radhi yake katika njia za salama, na huwatoa katika giza kuwapeleka kwenye nuru kwa amri yake, na huwaongoa kwenye njia iliyo nyooka.” [Al Maidah: 16]

Imeandikwa kwa Ajili ya Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir na

Said Bitomwa

Mwanachama wa Afisi ya Habari ya Hizb ut Tahrir Tanzania

Andika maoni

Hakikisha umejaza (*) habari zinazohitajika palipoashiriwa. Kodi za HTML haziruhusiwi.

rudi juu

Vifungu vya Tovuti

Viunganishi

Magharibi

Ardhi za Waislamu

Ardhi za Waislamu