Mnamo Jumamosi 27 Oktoba, kwa Baraka za Allah, Alhamdulillah, Kitengo cha Wanawake katika Afisi Kuu ya Habari ya Hizb ut Tahrir kwa ushirikiano na Hizb ut Tahrir / Wilayah ya Tunisia kwa ufanisi kilifanya kongamano kubwa na la kuvutia la kimataifa la wanawake jijini Tunis lenye kauli mbiu, “Familia: Changamoto na Suluhisho la Kiislamu” ili kuelezea sababu na suluhisho la Kiislamu juu ya mgogoro unaoathiri utulivu na umoja wa ndoa na maisha ya familia katika jamii kote ulimwenguni, ikiwemo biladi za Waislamu. Tukio hili muhimu lilihudhuriwa na zaidi ya wanawake 250 kutoka kote nchini Tunisia wakiwemo mawakili, walimu, walezi wa watoto, wahandisi, wanafunzi wa vyuo vikuu, viongozi wa jamii, na watetezi wa vijana. Hotuba zilitolewa na wanachama wa kike wa Hizb ut Tahrir kutoka Tunisia, Uturuki, Ardhi Iliyo Barikiwa – Palestina, Pakistan, Lebanon, Indonesia, Ghuba la Kiarabu. Uholanzi, na Uingereza. Kongamano hilo vile vile lilipeperushwa moja kwa moja mtandaoni kwa washiriki wa kimataifa na kutazamwa na maelfu ya watazamaji kutoka katika pembe tofauti tofauti duniani.