Mnamo Jumapili 17 Septemba, shirika la msaada la ‘Save the Children’ lilionya kuwa wakimbizi wa Rohingya nchini Bangladesh huenda wakafariki kutokana na uhaba wa chakula, makao, na bidhaa msingi za usafi. Zaidi ya Waislamu wa Rohingya 410,000 wamekimbia Myanmar na kwenda Bangladesh tangu Agosti 25 kutokana na kampeni ya mauaji ya halaiki inayotekelezwa na jeshi la Burma. Kwa mujibu wa shirika la UNICEF, asilimia 80% ya wakimbizi hawa ni wanawake na watoto, 92,000 kati yao wako chini ya umri wa miaka 5, na takriban wanawake 52,000 ni waja wazito au wananyonyesha.